News

Tume yakamilisha mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 3 vya Wilaya ya Kondoa

Tume yakamilisha mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 3 vya Wilaya ya Kondoa
Sep, 27 2018

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumzi ya Ardhi kwa kushirikiana na Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji (LIC) pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa imekamilisha upangaji wa matumizi ya ardhi ya vijiji vya Kwadelo, Boma ya Ng’ombe na Kilele cha Ng’ombe vilivyopo katika Wilaya ya Kondoa, Mkoani Dodoma.

Vile vile, Tume kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya pamoja na Halmashauri za Vijiji husika imewezesha upimaji wa vipande vya ardhi kwa ajili ya utoaji wa hati milki za Kimila kwa wananchi wa vijiji hivyo. Jumla ya vipande vya ardhi 1506 vimepimwa na hadi sasa (Septemba 27, 2018) jumla ya hati 990 za Haki Miliki za Kimila zimekwishaandaliwa. Upangaji wa matumizi ya ardhi na upimaji wa vipande vya ardhi katika vijiji hivyo ulianza Mwezi Julai 2018 na ulihusisha pia usuluhishi wa migogoro ya mipaka kati ya vijiji vya Kwadelo na Boma ya Ng’ombe ambapo wazee maarufu wa vijiji hivyo, viongozi wa dini, viongozi wa vijiji pamoja na wajumbe wa Halamashauri za Vijiji hivyo walihusika.

Ukamilishaji maandalizi ya hati unaendelea na unatarajia kukamilika mwanzoni mwa Oktoba 2018. Kukamilika kwa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji hivyo kunafanya idadi ya vijiji vyenye mipango ya matumizi ya ardhi kufikia 1816 kati ya vijiji 12,545 vilivyopo kote nchini.