Select Language:  ENGLISH   |   KISWAHILI

Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na Asasi ya Kiraia ya Care International, Tanzania, iliandaa mkutano wa siku tatu (3) wa Kikosi Kazi (Task Force) uliofanyika katika ukumbi wa Edema, Mkoani Morogoro tarehe 8-10/9/2016. Mkutano huu ulihusu utekelezaji wa makubaliano na mapendekezo yaliyotolewa wakati wa mkutano wa wadau wa upangaji, usimamizi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya Ardhi uliofanyika Morogoro tarehe 4-5/08/2016. Moja ya mapendekezo ya mkutano huu ilikuwa ni kuunda Kikosi Kazi kitakachoshughulikia utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na wadau katika mkutano huo. Hivyo, Tume ilifanya mawasiliano na Makatibu Wakuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi; Maliasili na Utalii na TAMISEMI ili kuteua Wajumbe wa Kikosi kazi hiki. Vile vile, Tume ilifanya mawasiliano na Asasi za Kiraia za Care International, Oxfam Tanzania, MVIWATA, Chama cha Wafugaji Tanzania, Ujamaa-CRT, na TNRF ili kupata wajumbe ambao waliungana na wale wa kutoka katika Idara na Taasisi za Serikali ili kuunda Kikosikazi.

Mkutano ulifunguliwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Dkt. Stephen Nindi na mwakilishi wa Asasi za Kiraia kutoka Care International Bi. Mary Ndaro. Wote kwa pamoja walisisitiza kuwa utatuzi wa changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ya Ardhi inayoendelea nchini ni jukumu la kila mdau wa Sekta ya ardhi. Hivyo, kwa kushirikiana pamoja kwa wadau wote katika uandaaji utekelezaji na usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi kutasaidia kupunguza migogoro ya ardhi nchini.

Malengo ya mkutano huo yalikuwa haya yafuatayo:

  1. Kupitia changamoto na mapendekezo yaliyoibuliwa wakati wa mkutano wa wadau na kuyapanga kulingana na vipaumbele na uzito wa changamoto au pendekezo.
  2. Kubainisha na kuandaa mikakati ya utekelezaji wa mapendekezo na kukabiliana na changamozo zilizoibuliwa.
  3. Kubainisha na kutambua Taasisi, Asasi za kiraia na mashirika yanayoshughulika na upangaji, utekelezaji na usimamizi wa mipango ya matumizi ya Ardhi nchini, kwa ajili ya kuandaa kanzi data
  4. Kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa mapendekezo yaliyoibuliwa katika mkutano wa wadau wa uadaaji, utekelezaji na usimamizi wa mipango ya Matumizi ya Ardhi nchini,
  5. Kuandaa mfumo wa uratibu na mawasilisano baini ya Wizara, Idara, Taasisi na wadau mbalimbali
  6. Kuandaa mpango wa elimu kwa umma juu ya masuala mbalimbali ya upangaji, utekelezaji na usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini
  7. Kuandaa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mpango kazi na utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini.

Mara baada ya kukamilika kwa kazi ya Kikosi kazi, hatua inayofuata ni kurejesha kwa wadau wote mpango kazi pamoja na mipango mingine ya elimu kwa umma, uratibu na mawasiliano pamoja na mpango wa tathmini na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mpango kazi ulioandaliwa

 

Joomla! Debug Console

Session

Profile Information

Memory Usage

Database Queries